Ijumaa 28 Agosti 2026 - 12:48
Bila Umoja wa Kiislamu, Umma Hauna Nguvu ya Kukabiliana na Uvamizi na Ubeberu

Hawzah/ Hujaatul-Islam Sayyid Ali Fahs, akichambua uzoefu wa Umoja wa Kiislamu, alisema: “Wazo lililoasisiwa na Imam Khomeini (q.s.) halikuwa wito wa kinadharia tu wa kuwaleta Waislamu karibu pamoja, bali lilikuwa ni mradi wa kiutendaji wa kukabiliana na uvamizi na ubeberu.”

Kwa mujibu wa taarifa ya Idara ya tarjama ya Shirika la Habari la Hawza, wakati ambapo wigo wa mashambulizi ya Marekani na Israel katika eneo unaendelea kupanuka, na migawanyiko ya ndani imekuwa miongoni mwa nyenzo kuu za kuizishinikiza jamii ya eneo hilo, Umoja wa Kiislamu unarejea tena kuwa katika kilele cha mjadala; si kama alama ya sherehe na maadhimisho pekee, bali kama suala linalohusiana moja kwa moja na uwezo wa Umma wa kulinda malengo yake na kukabiliana na maadui zake.

Katika zama ambazo Palestina inakabiliwa na uvamizi na kukiukwa heshima yake, huku nchi za eneo zikiwa katika hatari ya kushambuliwa na watu wake kulazimika kuhama makazi yao, swali kuhusu faida na ulazima wa umoja linaunganishwa na swali kubwa zaidi: Ingekuwaje iwapo uwezo mkubwa wa kibinadamu, kiuchumi na kisiasa ambao ulimwengu wa Kiislamu nao ungekusanywa pamoja kuangazia masuala yake ya msingi?

Hujaatul-Islam Sayyid Ali Fahs, Mkuu wa Kitengo cha Uhubiri na Shughuli za Kiutamaduni cha Hizbullah, amechambua uzoefu wa Umoja wa Kiislamu na kusisitiza kwamba, wazo lililoasisiwa na Imam Khomeini (q.s.) halikuwa wito wa kinadharia tu wa kuwaleta Waislamu karibu pamoja, bali ulikuwa mradi wa kiutendaji uliolenga kubadilisha mambo yanayowakutanisha Waislamu kidini kuwa nguvu ya kisiasa na kijamii katika kukabiliana na uvamizi na ubeberu.

Fahs, katika mahojiano na tovuti ya habari ya «Al-Ahed», huku akieleza kwamba: Palestina, Quds, Muqawama na kukabiliana na dhulma na uvamizi ni maeneo halisi ya kuupima uhalisia wa dhana ya umoja, alisema: “Umma wenye kiwango hiki cha uwezo na rasilimali hauwezi kubaki mateka wa mgawanyiko na kusambaratika. Kubadilisha umoja kuwa mwenendo na kitendo cha kila siku kunatosha kubadilisha mizani ya nguvu na kubadili namna ulimwengu unavyoshughulika na mataifa ya eneo.”

Umoja wa Kiislamu si jambo la muda au la kujitokeza kwa bahati

Sayyid Fahs, akisisitiza kwamba, Umoja wa Kiislamu si jambo la muda au la mpito kwa Umma, bali ni mradi halisi ambao juhudi zimewekwa katika kuuimarisha na kuugeuza kuwa mkakati wa kiutendaji, alisema: Imam Khomeini alitoa wazo la “Wiki ya Umoja wa Kiislamu” kwa kutegemea azma ya kuunganisha Umma kuangazia mambo yanayowakutanisha, badala ya kuruhusu tofauti ziwe sababu ya kugawanyika na kugombana.

Mjumbe huyo wa Hizbullah alisema: “Mambo yanayowakutanisha Waislamu, wawe Mashia au Masunni, ni mengi sana; yanaanzia katika Qur’ani Tukufu na Mtume Mtukufu (s.a.w.w.), na kufikia katika idadi kubwa ya imani, dhana na malengo ya pamoja ya Kiislamu.”

Aliongeza: “Kiasi cha mambo yanayowakutanisha Waislamu ni kikubwa zaidi kuliko maeneo ya tofauti zao; jambo linaloufanya Umoja kuwa chaguo linalowezekana na la lazima, hususan katika kivuli cha changamoto kubwa ambazo Umma unakabiliana nazo. Mambo yanayowakutanisha hayaishii katika masuala ya kidini na kiitikadi, bali yanaenea hadi kwenye masuala ambayo ni muhimu kwa Waislamu wote, na yanayoongoza ni Palestina, Quds, pamoja na kukabiliana na ubeberu duniani, Uzayuni, uvamizi na mashambulizi.”

Palestina inaonesha wazi gharama ya kutokuwepo kwa umoja

Sayyid Ali Fahs aliliweka suala la Palestina katika kilele cha masuala ambayo yangeweza kuwa msingi imara wa Umoja wa Umma. Anaamini kwamba kiwango ambacho Palestina inashuhudia leo cha uvamizi na ukatili wa Israel ambacho hakijawahi kushuhudiwa, kisingefikia kiwango hiki iwapo Umma ungeitumia kwa dhati dhana ya Umoja wa Kiislamu.

Alisema: “Suala la Palestina si suala la kundi, madhehebu au jumuiya fulani, bali ni suala linalowahusu watu wote, na la kibinadamu. Kuungana kwa Waislamu katika suala hili kungeweza kuongeza kiwango cha uwezo wao wa kukabiliana na uvamizi na kuunga mkono haki za watu wa Palestina.”

Alibainisha: “Umoja wa Kiislamu unaweza kuwa sababu muhimu zaidi katika kuratibu juhudi za Umma, wakati kutokuwepo kwa dira halisi miongoni mwa baadhi ya serikali, nchi, viongozi na taasisi za Kiislamu kumesababisha kudhoofika kwa uwezo wa kumtambua adui wa kweli.”

Anaamini kwamba miongoni mwa matokeo hatari zaidi ya kutokuwepo kwa dira hiyo ni kubadilika kwa vipaumbele, kiasi kwamba wakati mwingine mzozo unaelekezwa katika njia za ndani, badala ya juhudi kuunganishwa katika kukabiliana na uvamizi, ubeberu na mashambulizi.

Kinachotokea katika eneo ni matokeo ya mgawanyiko

Sayyid Ali Fahs ameunganisha hali ya mgawanyiko katika ulimwengu wa Kiislamu na mazingira ya umwagaji damu ambayo eneo hilo linashuhudia, kuanzia Ghaza hadi Lebanon, Syria na maeneo mengine ya kikanda. Anaamini kwamba ukubwa wa uvamizi, ukatili na uhamishwaji wa watu unaakisi sehemu ya matokeo ya Waislamu kutokuungana kuzunguka thamani zao za kiimani na malengo yao ya kimkakati.

Alisisitiza: “Iwapo Umma ungeungana kuzunguka masuala ya Palestina, Quds na kukabiliana na dhulma, ujeuri, Muqawama, uvamizi na uchokozi, ungekuwa katika nafasi tofauti kabisa na ungekuwa na uwezo mkubwa zaidi wa kuwazuia wavamizi na kuzilinda jamii zake. Tatizo haliko katika ukosefu wa uwezo, bali katika kutowekeza kwa pamoja katika uwezo huo ndani ya mfumo wa mradi mmoja uliounganishwa.”

Mabilioni ya Waislamu na rasilimali kubwa

Mkuu wa Kitengo cha Uhubiri na Shughuli za Kiutamaduni cha Hizbullah amezungumzia idadi ya watu katika ulimwengu wa Kiislamu, akieleza kwamba Umma huu unajumuisha zaidi ya Waislamu bilioni moja na, kwa mujibu wa baadhi ya makadirio, unakaribia kufikia Waislamu bilioni mbili. Aidha, una rasilimali nyingi za asili, uwezo mbalimbali, migodi, utajiri pamoja na rasilimali kubwa za kiuchumi na kibinadamu.

Anaamini: “Rasilimali hizi, iwapo zitatumika ndani ya mfumo wa mradi wa Umoja wa Kiislamu, zinaweza kuugeuza Umma kuwa nguvu yenye ushawishi katika ngazi ya kimataifa.”

Alisisitiza: “Kuunganisha uwezo wa kibinadamu, mali na uwezo mbalimbali kungebadilisha kwa msingi namna ulimwengu unavyoshughulika na Umma wa Kiislamu na mataifa ya eneo.”

Sayyid Fahs aliongeza: “Uwekezaji wa kweli katika uwezo huu ungeweza kupunguza ukubwa wa misiba ambayo Ghaza imeshuhudia, mawimbi ya uhamishwaji na mashambulizi ambayo Lebanon imekabili, pamoja na mashambulizi yaliyoikumba Syria na maeneo mengine ya Kiarabu na Kiislamu.”

Kwa hiyo, kwa mujibu wa Sayyid Fahs, umoja si tu kuwafanya Waislamu kuwa karibu wao kwa wao, bali ni mradi wa kujenga nguvu yenye uwezo wa kulinda maslahi yao na kubadilisha rasilimali zilizotawanyika kuwa nguvu ya pamoja yenye ushawishi.

Imam Khomeini (q.s.): Kutoka kwenye tofauti hadi kuwa jukwaa la kukutana na kuungana

Sayyid Ali Fahs, katika maelezo yake kuhusu uzoefu wa Imam Khomeini (q.s.), alisema: Mwanzo ulikuwa katika suala ambalo kwa mtazamo wa kwanza lilionekana kuwa ni tofauti; yaani, kuamua tarehe ya kuzaliwa kwa Mtume Mtukufu Muhammad (s.a.w.w.).

Wakati idadi kubwa ya wanazuoni wa Ahlus-Sunna na baadhi ya wanazuoni wa Shia wanaichukulia tarehe 12 Rabiul-Awwal kuwa ndiyo tarehe sahihi, idadi kubwa ya wanazuoni wa Shia na baadhi ya wanazuoni wa Ahlus-Sunna wanaamini kwamba tarehe ya kuzaliwa kwake ni 17 Rabiul-Awwal.

Alibainisha: Imam Khomeini (q.s.) hakulishughulikia tofauti hii kama tatizo ambalo lilipaswa kuondolewa au kufutwa, bali alijitahidi kuibadilisha kuwa fursa ya kuleta umoja.

Mjumbe huyo wa Hizbullah alisema: “Wazo hili lilijengwa juu ya msingi kwamba kila upande uhifadhi mtazamo wake kuhusu tarehe ya kuzaliwa kwa Mtume, lakini badala ya tofauti hiyo kugeuzwa kuwa sababu ya ugomvi na mzozo, kipindi kati ya tarehe 12 hadi 17 Rabiul-Awwal kikapewa jina na kupitishwa kuwa ‘Wiki ya Umoja wa Kiislamu’.

Kwa namna hiyo, eneo la tofauti likageuzwa kuwa jukwaa la kuungana na kukutana, ambapo Waislamu hukusanyika kuadhimisha kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Mtume Mtukufu (s.a.w.w.) na kujadili masuala, changamoto na mambo yanaousumbua Umma.”

Umoja si sherehe na mikutano pekee

Sayyid Ali Fahs alisisitiza: “Imam Khomeini hakutaka Wiki ya Umoja wa Kiislamu ibaki katika sherehe, hafla na mikutano pekee, bali alitaka iwe fursa ya kuyapitia upya masuala ya Umma na kuongeza uwezo wake wa kukabiliana na changamoto.”

Aliendelea: “Imam alihamisha dhana ya umoja kutoka katika uwanja wa fikra na nadharia na kuipeleka katika uwanja wa vitendo. Kwa hiyo, suala hilo halikuhusu tena mikutano ya kiutamaduni na kiakili au mikusanyiko ya kielimu pekee, bali lilipaswa kuwa kitendo ambacho jamii za Kiislamu zinakiishi.”

Alisema: “Imam Khomeini (q.s.) alitaka umoja uwahusishe wanazuoni wa Kiislamu, wasomi na viongozi wa kiutamaduni, na kisha uhamishwie kwenye taasisi na matabaka mbalimbali ya Umma, hatimaye ufikie katika harakati na mikondo wa wananchi katika jamii za Kiislamu.”

Muqawama ni sehemu ya umoja

Sayyid Ali Fahs anachambua dhana na istilahi muhimu ambazo Imam Khomeini (q.s.) alikusudia kuziunganisha na mradi wa Umoja, miongoni mwa hizo ikiwa ni suala la Muqawama na kukabiliana na uvamizi.

Alieleza: “Historia ya Umma imeshuhudia juhudi za mara kwa mara za ukoloni na zana zake za kuchochea vita vya kiutamaduni na kidini kwa lengo la kuisambaratisha jamii na kudhoofisha uwezo wake wa kukabiliana na mvamizi. Kwa hiyo, Muqawama hauwezi kutenganishwa na Umoja wa Kiislamu, kwa sababu Muqawama unahitaji kuunganisha juhudi za Umma, wanazuoni, wasomi, viongozi wa kiutamaduni na vijana wake kuangazia masuala ya msingi.”

Alilitaja Palestina kuwa mfano ulio wazi wa jambo hili na kusisitiza: “Kulilinda hakupaswi kuhusishwa na swali la madhehebu ya wakazi wake, bali linapaswa kuangaliwa kama suala la kudai haki na kama jambo la Kiislamu na kibinadamu.”

Kuilinda Palestina ni jukumu la Kiislamu

Sayyid Ali Fahs alisisitiza: “Waislamu wanaofuata Madhehebu ya Ahlul-Bayt (as), kama Waislamu wengine, wana wajibu wa kuilinda Palestina, bila kujali kama Mashia wapo au hawapo huko.”

Alisema: “Watu wengi wa Palestina ni Ahlus-Sunna, lakini jambo hili halifanyi suala la Palestina kuwa suala la Kisunni pekee; kwa sababu kumlinda Mwislamu ni wajibu wa ndugu yake Mwislamu, kama ambavyo kuilinda kila sehemu ya Umma ni jukumu la Waislamu wote.”

Alisisitiza: “Mwislamu wa Shia anapomtetea ndugu yake Mwislamu wa Sunni, mshindi wa kweli ni Uislamu na Waislamu, na kinyume chake. Wakati huo huo, katika tofauti na mgawanyiko hakuna mshindi wa kweli. Kwa sababu hiyo, umoja hugeuka kuwa kitendo halisi pale Mwislamu anapotambua kwamba masuala yanayomsumbua ndugu yake ni masuala yanayomsumbua yeye mwenyewe, na kwamba kulengwa kwa sehemu yoyote ya Umma ni tishio kwa sehemu nyingine za Umma.”

Sera ya kuugawa Umma vipande vipande na kulenga makundi moja baada ya jengine

Sayyid Ali Fahs alionya kuhusu mkakati unaotegemea kulenga kundi au dhehebu fulani moja moja na mvamizi, ukoloni au mradi wa Marekani na Israel, kwa kisingizio kwamba Waislamu wengine hawatalengwa.

Alisisitiza: “Mtazamo huu si sahihi, kwa sababu adui anapoelekea kuikandamiza sehemu moja ya Umma kwa namna ya pekee, haimaanishi kuwa ameziacha sehemu nyingine. Uzoefu wa kihistoria umethibitisha kwamba kuugawa Umma hufanywa kwa hatua, kwa kulenga kundi moja na kisha kuhamia katika kundi jingine.”

Alibainisha: “Baadhi ya madola ya kimataifa yanaweza kutoa lugha tofauti kwa baadhi ya harakati au kuwapa ahadi na manufaa ya kisiasa, kwa lengo la kuwaathiri au kuwatenganisha na sehemu nyingine za Umma, kabla ya kuanza kuwalenga wengine.”

Anaamini kwamba sera hii, kwa asili yake, inalenga kuligawa eneo vipande vipande na kuyazuia mataifa yake kuchukua msimamo mmoja dhidi ya uvamizi na miradi ya kikoloni.

Umoja ni jukumu la wanazuoni, wasomi na vijana

Sayyid Ali Fahs alieleza: “Imam Khomeini (q.s.) alilenga kuutoa umoja kutoka katika mfumo wa watu wasomi na kuupeleka kwa jamii nzima, kiasi kwamba usibaki kuwa jukumu la wanazuoni, wasomi na viongozi wa kiutamaduni pekee, bali uwe sehemu ya ufahamu na mtazamo wa vijana, harakati za wananchi na mwili wa jamii ya Kiislamu.”

Alisisitiza: “Vijana ni kundi kubwa zaidi na lenye uwezo mkubwa zaidi katika kujenga mustakabali. Kwa sababu hiyo, wanapaswa kuuelewa Umoja wa Kiislamu kama jambo la kiutendaji na halisi, si kama kaulimbiu ya msimu na ya muda inayowekwa tu katika wiki moja au kwenye tukio maalumu.”

Aliendelea: “Umoja ni miongoni mwa nguzo za nguvu ya Umma, na kuushughulikia kwa namna hii kunaufanya utoke katika kuwa kaulimbiu na kuwa nguvu halisi yenye ushawishi katika hali halisi.”

Umoja: Njia ya kurejesha nguvu ya Umma

Katika muhtasari na hitimisho la mtazamo huu, Sayyid Fahs alisisitiza: “Umma wa Kiislamu una vipengele vya nguvu za kibinadamu, mali na uchumi, lakini unahitaji mfumo mpana utakaowezesha uwezo huo kutumika katika kuhudumia masuala na malengo yake ya msingi.”

Anaamini: “Umoja wa Kiislamu ukigeuzwa kuwa mtazamo na mwenendo wa kiutendaji, unaweza kupanga upya vipaumbele vya Umma na kuelekeza uwezo wake, badala ya kuteketea katika tofauti za ndani, kuelekea katika kukabiliana na uvamizi, ubeberu na ukosefu wa haki.”

Alisisitiza: “Kile ambacho Imam Khomeini alikusudia kuhusu umoja hakikuwa tu kuwakusanya Waislamu katika matukio mbalimbali, bali ni kujenga uelewa wa pamoja ambao utafanya kila sehemu ya Umma ihisi kwamba masuala ya sehemu nyingine ni masuala yake pia. Kwa hiyo, Mwislamu anapoitetea Palestina kwa sababu ni suala la haki; anapoona uvamizi dhidi ya sehemu yoyote ya Umma kuwa ni uvamizi dhidi ya wote; na pale uwezo wa wanazuoni, wasomi, viongozi, vijana na mataifa unapounganishwa kuzunguka masuala ya kimkakati, ndipo Umoja wa Kiislamu unapogeuka kuwa nguvu ya kweli ya kisiasa na kijamii.”

Kwa msingi huo, Sayyid Ali Fahs alihitimisha kwamba kukabiliana na miradi ya Marekani na Israel hakuanzi tu kwa kuwa na vipengele vya nguvu, bali huanza kwa uwezo wa kuzikusanya na kuzitumia ndani ya mfumo wa mtazamo na dira moja. Kwa sababu Umma unaoungana kuzunguka masuala yake ya msingi utakuwa na uwezo mkubwa zaidi wa kulinda watu na mali zake, na uwezekano wa kugawanywa, kutengwa na kugeuzwa tofauti zake kuwa nyenzo zinazowahudumia maadui wake utakuwa mdogo zaidi.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha